Blog

Maoni Ya Mwana-Buhigwe Na Ustawi Wa Kigoma

Maoni Ya Mwana-Buhigwe Na Ustawi Wa Kigoma

Pongezi nyingi, Mhe. Dr. Philip Mpango, kwa hatua ya kupewa nafasi kugombea uongozi, ngazi ya Ubunge, kwa ajili ya jimbo letu la Buhigwe, kupitia chama tawala. Mpaka hatua hii inapendeza kwamba umeaminiwa na wengi na kuonekana unafaa kuwaongoza wana-Buhigwe, na zaidi sana kuwawakilisha hatimaye katika Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania – Mungu akipenda.

Kwa kuwa mimi ni mwana-Buhigwe, na kwa bahati ndugu yako wa karibu, napenda kukushirikisha maoni yangu kuhusu nini kinaweza kufaa kwa ajili ya Buhigwe, nawe ukaonekana kweli kuwa jibu [au walau kuwa na mchango] kwa matumaini waliyonayo watu wa Buhigwe, kuhusu maisha yao na jinsi yanavyoweza kuboreshwa. Hapa naorodhesha kwanza Fursa zinazopatikana Buha yetu, na pili, Matatizo makubwa ninayoyaona: 

I: Fursa katika Buha:

  1. Nguvu-kazi Vijana, na hata watu wazima
  2. Moyo wa Waha Kujituma na kufanya kazi – tangu zamani
  3. Hali ya kuwa Mpakani na Burundi
  4. Kupatikana bado kwa Vilima, Mabonde na Ardhi nzuri kwa Kilimo n.k.
  5. Hali ya hewa na Upatikanaji Mvua
  6. Amani na Utulivu mpaka sasa – tofauti na Jirani…
  7. Miundombinu inayopatikana mpaka sasa

 II: Matatizo yanayoikabili Buha yetu

  1. Shida ya Mawasiliano na Usafiri
  2. Shida ya Elimu na Fursa za Masomo
  3. Shida ya Huduma za Afya
  4. Shida ya Lishe Duni
  5. Shida ya Mazingira na Upatikanaji wa Maji
  6. Shida ya Uongozi ngazi ya Vijiji
  7. Shida ya Huduma ya Maafisa na Wataalam wa Serikali
  8. Shida ya Ukosefu wa Mang’amuzi, Ubunifu na Moyo wa Ujasiriamali
  9. Shida ya Ukosefu wa Moyo wa Kusaidiana
  10. Shida nyinginezo

 

Tuseme kwanza kuhusu Fursa zinazopatikana katika Buha yetu:

  1. Kuhusu Nguvu-kazi, Vijana na Watu wazima, nalenga kusema juu ya wingi wa watu [population] ya Wana-Buhigwe, wengi wa wakazi wakiwa Vijana. Mpaka hivi karibuni tulikuwa sehemu ya Wilaya ya Kasulu ambayo iliongoza muda mrefu kwa wingi wa watu katika Wilaya za Mkoa wa Kigoma. Hata baada ya kumegwa na kuwa Wilaya ya kujitegemea, twaweza kusema tuna wakazi wengi ambao tukiweka nguvu yetu katika shughuli za maendeleo tunaweza kupiga hatua kubwa. Wingi wetu unatusaidia kutengeneza soko kubwa ambamo tunaweeza kuuziana vitu, sisi kwa sisi, pia kubwa wa soko unashawishi wengine kutuletea bidhaa zao pia. Wingi wetu unatuongezea uwezo wa kupeana mawazo na msaada katika shughuli mbalimbali. Palipo na wengi ubunifu ni mkubwa zaidi pia.
  2. Tangu zamani Waha tunafahamika kama watu wa kazi, wenye nguvu na bidii katika kazi hata zinazowashinda wengine, japo wakati fulani, labda hata sasa sifa yetu hii imetumika vibaya, mfano katika U-MANAMBA. Wajibu wetu sasa ni kuidumisha sifa hii njema; kuikuza na kuwarithisha Watoto na wajukuu wetu. [Labda walimu wa Nidhamu na Maadili shuleni wanaweza kuona namna ya kuijumuisha katika mitaala / mazungumzo yao; au Viongozi wa Siasa kujipa muda kutembelea shule zetu na kuongelea mambo ya jinsi hii.]
  3. Hali ya kuwa Mpakani na Burundi inatupatia fursa ya kujifunza mengi; mfano, wenzetu wanatuzidi nini tunachoweza kuiga? Warundi ni wachapa-kazi, labda kuliko Waha. Ndio maana tumekuwa tukiwatumia kwa ajira mbalimbali, hasa kilimo, ujenzi, n.k. Nchi jirani inatuongezea soko tunakoweza kuuza bidhaa zetu. Jirani hawa wanatuuzia sana Maparachichi [kwa mfano]. Basi tujifunze na sisi kuyalima, au tuyachakate na kuongeza ubora wa thamani na tuwauzie Watanzania wenzetu, au Burundi kwenyewe, au nchi nyingine [Mafuta, unga wa mbegu, n.k.]
  4. Vilima na Mabonde ya Buha yanaipamba sana Buha yetu. Wale tuliopata bahati ya kusafiri huku na kule tunajua. Vyote, mabonde na Vilima pia, vinafaa kwa kilimo na Ufugaji. Inategemea tu tunatengaje maeneo yetu. Ardhi yetu ina rutuba kuliko sehemu nyingi za nchi yetu. Kazi yetu si kuitumia tu kuzalisha mali, bali pia kuitunza na kuiboresha, maana hatari ya Uharibifu inaanza kuonekana dhahiri. Gisozi, Muharuro, Kabuye [?], Gipfizi, Gishigwe, Cheya n.k. ni vilima vinavyopamba Buha yetu, na hivyo pia tuna Muyovozi, Malagarasi, Kigombe, Rugambwa, Mutunguruzi, Ruchugi, Mulangirizi, Mukoza [?] ambayo ni baadhi ya mito yetu yenye mabonde mazuri. Tunaweza kutengeneza mabwawa ya samaki, Bustani, n.k.
  5. Hali ya Hewa na Upatinaji wa mvua si mbaya kulinganisha na sehemu nyingine za Tanzania. Mgawanyiko wa Masika na Kiangazi unatupatia fursa ya kupanga vizuri shughuli zetu za uzashaji na muda wa kupumzika; mazao ya kutegemea mvua na yale ya kutegemea umwagilizaji mabondeni, na kadhalika. Hali ya hewa Buha inaturuhusu kulima mazao ya aina nyingi kabisa: Kahawa [hata Chai ingestawi], Migomba, mahindi na Maharage; Viazi na Mihogo; Karanga, Mbaazi, na pia matunda kama Machungwa, Maparachichi, Nanasi, Malimau, Maembe, na kadhalika. Sifa hizi za Buha, hasa ukijumuisha na ardhi nzuri na undongo wenye rutba, zinapafanya patamanike kwa wageni na wawekezaji. Tujifunze namna ya kuishi nao kwa faida yetu na wao.
  6. Hali ya utulivu tuliyonayo mpaka sasa tuitumie vizuri kupanga maisha yetu vizuri. Tumshukuru Mungu na tumwombe aendelee kutupa busara ya kuilinda na kuidumisha. Tumshukuru Mungu pia kwa moyo aliotujalia kuwasaidia wenzetu jirani, waliokimbilia kwetu mara kadhaa amani ilipokuwa shida kwao. Amani itatupatia utulivu kufanya shughuli za uzalishaji.
  7. Tunayo miundo-mbinu mbalimbali: Barabara, umeme, Maji ya bomba na taasisi za Afya na Elimu, japo si kwa kiwango tunachoweza kutamba sana. Hata hivyo tunatumia kwa sasa hicho kilichopo, wakati tunajipanga kuboresha na kuongeza miundombinu hiyo…

 Kuhusu Matatizo Yanayoikabili Buha Yetu

  1.  Shida ya Usafiri: Tunatambua kuwa barabara zetu kadhaa zilichongwa na Wakoloni, na nyingine si haba zilianzishwa na Wamisionari. Hizi nyingi zilikuwa zinatusaidia sana hasa Kiangazi. Wakati wa Masika zilipitika kwa shida kubwa, na mara nyingine madaraja yalileta shida. Baadaye Serikali yetu imerithi shughuli ya utunzaji barabara na madaraja, na kwa sasa tunaona vile ambavyo kumekuwa na mabadiliko makubwa kwa baadhi ya barabara zetu kuchongwa kila mwaka na hata kuwekewa changarawe/ kifusi. Mpaka sasa kuna vijiji jirani ambavyo haviunganishwi na barabara yoyote. Nawaza, kwa mfano, kati ya Kasumo na Kajana; Kasumo na Munyegera; na labda sehemu nyingine [sina hakika na Buhoro na Katundu]. Kadiri tunavyorahisisha mawasiliano kati ya vijiji, vivyo hivyo inaweza kukuza uzalishaji na masoko kati yetu.
  2. Shida ya Elimu na Fursa za Masomo: Ni bahati kwamba siku zetu hizi kuna Shule za Msingi kila Kijiji, au hata mbili, tatu, kadiri ya ukubwa wa Kijiji na wingi wa watu. Vijiji vingine vina bahati ya kuwa na shule ya Sekondari, au vijiji kadhaa vinachangia shule, kama Shule ya Sekondari Muyama kwa ajili ya Muyama, Kalege na Kasumo, na nadhani Biharu na Kajana pia.
  • Shule zetu nyingi zinakosa vifaa muhimu [madawati, vitabu, walimu, n.k.]
  • Matokeo yake ni kwamba bado asilimia ya Watoto wetu wanaopata nafasi ya kuingia Sekondari ni ndogo [?]. Wanafunzi wanaomaliza darasa la 7 wengi hawaendelei na Sekondari kwa sababu shule hizo ni chache. Tungepashwa kuwa na Sekondari kila Kijiji.
  • Je, kwa Kata ya Kajana, au Tarafa ya Muyama, asilimia ngapi ya wahitimu wa darasa la 7 wanaingia sekondari?
  • Kuna faida kwa shule 2, 3 za msingi kuwa pamoja/ karibu: Vifaa kadhaa, majengo na hata walimu, vinaweza kutumika kwa pamoja [sharing / pooling of resources]. Lakini kuna hasara pia: hatari wakati wa milipuko ya magonjwa kama Kipindupindu, Corona, n.k.; Ugumu wa kutunza nidhamu na ugumu wa kujenga Sifa za shule husika [upekee] kwa kujitegemea. Uwezo wa kujitanua na kufanya shughuli za maendeleo na hata michezo, unapungua.
  1. Shida ya Huduma za Afya: Huduma za Afya, kama vile Elimu, zinakuwa bado si za kuridhisha sana sababu uwezekano wa kumfikia daktari mwenye ujuzi katika fani fulani, ni mdogo. Ingekuwa vema kuwa na Kituo cha Afya walau, kila Kijiji, japo juhudi mpaka sasa ni kuwepo kimoja kwa kila Kata. Ingewezekana kujenga walau “Maternity Ward” kwa kila Zahanati.
  • Serikali ingekazania Utafiti wa Dawa za Asili nadhani ni jambo zuri, na wale wanaofahamu dawa za asili wahamasishwe kushirikisha wengine elimu yao.
  • Zahanati na Vituo vya Afya vitoe pia Elimu ya Afya kuliko tiba tu.
  1. Shida ya Lishe Duni: Ni rahisi kupata mlo wenye wanga wa kutosha katika milo yetu Buha, lakini tuna shida kupata Protini na Vitamini. Protini ya Maharage, Kunde, Mbaazi, Karanga, n.k., ni nzuri, lakini nyongeza toka Dagaa, Samaki na Mayai ingeongeza upatikanaji wa “Calcium” na viinilishe vingine. Waha tunapungukiwa sana matumizi ya matunda, na hivi tunajinyima sana Vitamini. Tunadhani matunda ni chakula cha Watoto na ndege. Lakini Mapera, Mapapai, Nanasi, Machungwa, Avocado, na Ndizi ni matunda ambayo tunaweza kuyapata kwa urahisi tukiamua. Hata “Inkeli,” ni matunda tunayoelekea kuyabeza. Nadhani pia hatutumii mboga za majani kwa wingi yakutosha.
  • Kuna umuhimu wa kuhimiza matumizi ya vyakula vyetu vya asili kama mtama, ulezi, majimbi, viazi vikuu, “Inumbu,” hata “Amatugo” n.k
  • Hatuna ubunifu katika kutengeneza milo yetu. Tunapika vyakula vyetu kwa namna ileile vizazi na vizazi, kumbe ubunifu kidogo unaweza kukoleza uzuri wa vyakula vyetu na kufanya hata “Amatugo” kupendwa.
  • Kuna haja ya kuboresha majiko yetu: yaweze kutumia kuni kidogo; kupika vyungu viwili - vitatu kwa mpigo, na kumwezesha anayepika kusimama kuliko kukaa au kuchuchumaa!
  • Tunashinda juani muda mwingi, na kazi zetu nyingi ni za kutoa jasho. Je, tunakunywa maji ya kutosha? Miili yetu inaumizwa sana kwa kukaa muda mrefu bila kuwa na maji ya kutosha! Jambo hili halisisitizwi yakutosha.
  • Tunakula kwa kuchelewa mno usiku! Kula saa 3, au saa 4, na kulala saa 5 usiku, tumbo limejaa, ni jambo lenye madhara makubwa kwa afya zetu!
  1. Shida ya Uharibifu wa Mazingira: Shida hii ni kubwa, hasa kwa kuwa ni matokeo ya shughuli za watu katika kutafuta riziki, na madhara ya shughuli zao hayaonekani moja kwa moja, bali hukua polepole. Kwa sababu ya shughuli za kutafuta kuni kwa upishi wa chakula, miti ya ujenzi wa nyumba zetu, na kazi nyingine, misitu na mapori yetu vimepotea kabisa. Uwindaji holela na haramu umefanya tusiwe tena na Sungura wala Paa, Swala, n.k. Buha yetu ilipendeza sana kwa miti, nyasi na mito iliyotiririka mwaka mzima karibu kila bonde. Hapo nyuma kidogo usingetembea maili 5 bila kuvuka mto wa uhakika. Leo karibu tunafanana na Ugogoni na Usukumani. Tulikuwa na mabwawa makubwa, mfano pale karibu na vijiji vya Muyama, Biharu na Nyamugali: Ilikuwa kawaida kukuta “Imisambi” ikicheza. Leo hii Watoto wetu hawajui “Imisambi” ni kitu gani. Maeneo yetu mengi yamebaki “amakungu” sababu ya ufugaji holela, na ndio sababu watu walianza kuhamia maeneo mengine hata kabla ya Vijiji vya Ujamaa!
  • Maisha ya Kijiji yakiwa na mpangilio, kuliko kufanya mambo holela, na kila huyu kadiri atakavyo, itatusaidia kuepuka madhara ya kimazingira.
  • Kwa uzoefu na Utafiti wa mahali pengine, inawezekana kurekebisha baadhi ya makosa yaliyokwishafanyika, mfano kuhuisha vyanzo vya mito na vijito vilivyokauka kwa kuepuka matumizi ya mabondeni yasiyo na mpangilio; kupanda miti ifaayo [Imigoti, Imiziguzigu; Imikuyu; Imiyovu, n.k.].
  • Je, si inawezekana kila kijiji kikawa na msitu wake, na kuongeza ekari walau 5 kila mwaka? Misitu ni akiba na rasilimali ya pekee kabisa. Raia wahamasishwe kuwa na miti yao ya matunda. Serikali isaidie uwepo wa vitalu vya miti kama ilivyofanya hapo nyuma!
  • Tuna shida kubwa sana ya mioto, na uchomaji holela wa majani, vichaka na misitu yetu! Wachungaji wa Kondoo, Mbuzi na Ng’ombe wanahusika sana na hili. Lazima wakemewe sana, waonywe – Watoto kwa watu wazima. Watoto wakatazwe kutembea na viberiti, lakini hasa wafundishwe kupenda mazingira, na zaidi sana waelekezwe / wasaidiwe vipi mifugo yao itapata malisho hasa Kiangazi! Wakulima pia wanahusika. Mara nyingi mioto inawatoroka wanapoandaa mashamba. Wengine eti wanafukuza panya na nyoka. Tutafute nyia nyingine.
  • Wataalam wetu watufundishe kulima kwa Matuta-Kingamo [terraces] ili kudaka maji na kuyazamisha ardhini [kuliko kuyaacha kutiririka na kutengeneza makorongo [kama Ntigwivumbura, Imanga ya Kamana…] na yakizama yakasaidia kudumisha vyanzo vya mito.
  • Tabia na mazoea ya kuua samaki kwa kutumia sumu ipigwe marufuku! Watu [vijana] wafundishwe na wahamasishwe kutengeneza mabwawa ya kufuga samaki mabondeni.
  1. Shida ya Uongozi wa Vijiji Vyetu: Viongozi wetu wengi hawajiamini, au hawajui wajibu wao ni nini. Wengine hawajui mipaka ya vijiji vyao; wengine hawajui wafanye nini na wageni wanaovamia maeneo yetu, au ni wepesi wa kuhongwa kwa kuwa hawajui madhara ya wavamiaji wanaonyemelea maeneo yetu. Wengine hawajui “thamani” ya ardhi yetu. Viongozi wengi ni wale wanaosubiri tu maelekezo kutoka ngazi za juu nini wafanye, au wawaambie wananchi, lakini wao wenyewe hawana mawazo wala ubunifu kabisa. Hata barabara ikiharibika katika maeneo yao kiasi wanachoweza kurekebisha, wanasubiri mpaka uongozi wa Wilaya ufanye kitu!
  • Nawaza ni viongozi wachache sana wamejishughulisha na kupanga na kutenga maeneo kwa shughuli mbalimbali za vijiji vyao: mfano akiba ya miti na misitu kwa shughuli mbalimbali; kilimo, ufugaji; kulinda vyanzo vya mito na mbwawa, n.k.
  • Uongozi wao ni kusubiri watu wawapelekee shida zao, kuliko kukagua kwa mfano uwepo na matumizi ya vyoo; kuhamasisha vijana kufanya kazi, kuliko kushinda kijiweni kupiga gumzo; kutambua kama kuna mtu au familia wanahitaji msaada fulani wa pekee, n.k.
  • Shida ya Masoko ya Usiku, na madhara yake kwa maadili ya vijana wetu, limetushinda kabisa! Je, tumenyoosha mikono?
  1. Shida ya Huduma za Wataalam wa Serikali: Mara nyingi tunajua au tumesikia kuwa kuna wataalam wa Kilimo, Misitu, Mifugo, na kadhalika. Uzoefu unaonesha kuwa wengi wao wanabaki katika ofisi zao za Wilaya, na wananchi hawanufaiki chochote na utaalam wao. Kwa kiasi fulani wale wa Mifugo tunawaona wataalam wa ngazi ya Kata, lakini wa Wilayani “they have no impact on village life!” Miti yetu ya matunda, mfano Machungwa, na Migomba, na mara kadhaa mazao kama Mahindi, Maharage, hushambuliwa na magonjwa au wadudu waharibifu. Wakulima wenyewe ndio wanahangaika kuulizia madukani, kana kwamba wenye-maduka ndio wataalam wetu! Hatuoni wataalam wakienda vijijini kuwaelekeza wananchi namna ya kufuga nyuki [kwa mfano], au kufuga samaki, mpaka mkulima mmoja-mmoja ahamasike mwenyewe kuwafuata. Inawezekana shida ni mfumo wa Serikali nzima tangu inapowaajiri, na “terms of employment.” Je, inawezekana wakawa na mahusiano zaidi na wananchi?
  • Ningetamani kuona wataalam wetu wana mashamba au walau bustani ndogo za mfano, ikiwezekana kila Kijiji. Wataalam wa Misitu na nyuki ndio wangekuwa na mizinga ya Nyuki, kuwaonesha wananchi namna ya kufuga. Hawa wangesimamia bustani za Miti na mbogamboga. Sisi mashamba-darasa tunayasikia kwingine tu!
  • Kama haiwezekani kuwa na miradi midogo ya mfano / mafundisho kila kijiji, ingeweza kufanywa sehemu walau chache na wananchi wakajulishwa na kualikwa kwenda kujifunza – Bustani ya Miti Kasumo, Ufugaji Nyuki Kilelema, Mabwawa ya Samaki Nyamugali, n.k.
  • Vyuo vinavyotuzunguka, mfano Sekondari zenye michepuo maalum, Chuo cha Kilimo Mubondo, vina mahusiano yepi na Wananchi wanaokuwa jirani? Je, hawana namna ya kupanua elimu wanayoitoa darasani ikawafikia na kuwafaidia wananchi jirani kwa semina/ warsha, au kuwasaidia upatikanaji vifaa, kama mbegu bira na miche bora…?
  • Serikali ifikirie kuwa na Kituo cha Zana za Kilimo kila Kata: kwa kuwa Watanzania wengi hujihusisha na Kilimo, tutapiga hatua haraka ikiwa nyenzo muhimu kama matrekta na matrela / magari ya kubebea mazao yatapatikana, hata kama yatakuwa ya kukodi. Usalama wetu utaletwa na uwezo wa kuongeza ukubwa wa mashamba yetu, na kuzalisha zaidi; kuwa na masoko na kufundishwa kuchakata mazao yanayoweza kuchakatwa ili kuongeza ubora wa thamani yake, kabla ya kuyafikisha sokoni. Vituo hivyo vinaweza pia kuwa na mashine za kukamua Mafuta ya Karanga; Alizeti, n.k., au kusaga mihogo / mahindi na kufunga Unga katika mifuko, kuliko kuuza mihogo na mahindi yenyewe.
  1. Shida ya Ukosefu wa Ubunifu na Moyo wa Ujasiriamali: Moja ya shida kubwa kabisa inayotukabili Buha, ni matumizi mabaya ya Rasilmali Muda! Hatuna mpangilio katika maisha yetu, na matokeo yake ni kwamba muda mwingi unapotea bila ya kuzalisha chochote! Shida nyingine kubwa ni kwamba hatuko wepesi wa kutambua fursa zinazotuzunguka, na hivyo tumekuwa wepesi wa kwenda kuwafanyia kazi wenzetu mikoa mingine na hata vijiji vingine. Ni kweli kwamba mara nyingine tunakatishwa tamaa na vitu vingi, mfano ukosefu wa masoko baada ya kuzalisha; ukosefu wa mvua; ukosefu wa pembejeo na nyenzo za kufaa, na labda kukosa mtaji, japo hata mtaji wa nguvu zetu hatuutumii yakutosha.
  • Kwa kuwa utambuzi wa fursa na rasilmali zilizopo vinaweza kuhitaji utaalam wa namna fulani, basi wataalam wetu wa Wilayani na Mkoani wawasaidie wananchi kuona wanaweza kufanya nini na kuzalisha vipi mali.
  • Wananchi, hasa vijana wasaidiwe kupanga muda katika shunguli za kuzalisha. Hii ina maana kuwa wawe na malengo mahususi. Kila mmoja awe na Ratiba ya muda mrefu na muda mfupi wa kazi, la sivyo maendeleo yataendelea kuwa ndoto!
  • Serikali za Vijiji ziwe na mamlaka ya kufuatilia ratiba na malengo ya kila kaya, na takwimu za malengo hayo [na utekelezaji wake ukifuatiliwa] zihifadhiwe katika ofisi ya Kijiji, hivi kwamba Mtendaji wa Kijiji akiulizwa, mwisho wa mwaka, anaweza kujua mwaka huu Kijiji cha Kasumo kilitarajia kuzalisha tani 12 za Maharage tokana na kaya 450 ambazo kwa ujumla zimelimwa ekari 18 za zao hilo mwaka 2020, na matokeo yake kumekuwa na nyongeza au upungufu [nakisi] kwa sababu hizi… Tukifikia hali hiyo tutakuwa tunapiga hatua madhubuti kuelekea maendeleo!
  • Uwezo wa kujiandalia ratiba ya kazi; kupanga malengo ya maisha na ubunifu, na pia namna ya kutambua fursa zinazokuwa katika maeneo anayoishi binadamu ni elimu inayoweza kufundishwa darasani. Ningeshauri kuwa elimu hiyo ianze Shule ya Msingi, ili vijana wanaohitimu shule-msingi wawe na kiasi cha elimu hiyo muhimu.
  • Serikali za Vijiji zenyewe ziwe pia na malengo fulani mahususi ya kila mwaka, mfano kuwa na Msitu wa miti, au Mizinga ya Nyuki, n.k., kwa malengo yanayojulikana, na kila mwaka wajue wanaipanua kiasi gani. Ina maana kuwa kuwe na mali za Kijiji tofauti na pesa “mfukoni” kwa mweka hazina wa Kijiji au Benki. Kama Serikali ya CCM inadai nchi / siasa yetu ni ya Kijamaa, basi Ujamaa huo uonekane katika nguvu na mafaa ya pamoja hata kwenye ngazi ya Kijiji.
  • Vijiji viwe na Maktaba ambapo panaweza kuwekwa mashapisho kuhusu elimu anuai. Vijitabu na Vitabu vingeweza pia kutunzwa humo kwa watu kujisomea, kuliko kutumia muda kila siku kilabuni. Lazima pawe na juhudi mahususi kubadili fikra za watu, na namna yao ya maisha. Maktaba hizo zinaweza kuambatana na kumbi zitakazotumika kama mahali pa mafunzo, kwa Video, Senema na kimafunzo, au mikutano na wataalam wanapoeleza /fundisha jambo.
  1. Shida ya Ukosefu wa Moyo wa Kusaidiana: Zamani, kabla mkoa wetu haujahusishwa katika zoezi la Vijiji vya Ujamaa, watu waliishi mbalimbali kulinganisha na wakati huu. Hata hivyo, watu waliweza kualikana na kusaidiana shughuli za Kilimo, Ujenzi wa nyumba na shughuli nyingine, hasa misiba na harusi. Ungetegemea kwamba sasa kwa kuwa tumekuwa karibu zaidi tutasaidiana kwa wepesi zaidi katika shughuli zetu, lakini kinyume chake moyo huo, japo upo kwa kiasi fulani, umepungua sana! Natamani kama tungesaidiana zaidi, mfano kumchangia mwenzetu akifikwa na maafa fulani, au hata akipata mahitaji muhimu ya kusomesha mtoto. Tuone kuwa isiwe tu rahisi kusaidiana katika shamrashamra za arusi, na labda kuzikana, lakini tuone pia umuhimu wa kupigana jeki hata wakati wa magonjwa na wakati wa hitaji la kuelimisha mwana.
  • Uongozi wa Kijiji uwe na takwimu kuhusu idadi ya walemavu – aina ya walemavu na mahitaji yao. Pawepo na takwimu za Wazee na mahitaji yao. Takwimu hizo zichochee mipango ya kuwasaidia.
  1. Shida nyinginezo: Ninatamani viongozi wetu wa Vijiji wawe ni watu wenye muono wa kimaendeleo. Mfano waone ni wanakijiji wangapi bado wanaishi kwenye nyumba za nyasi, na tutahitaji miaka mingapi kuondokana na hali hiyo Kijiji husika – kwa mipangilio ipi!

 Nyongeza – Taarifa

 Natengenezesha ramani ya maeneo yetu ili kuonesha vilima, mito na vijito vilivyo karibu na eneo la Kasumo, ikiwezekana Kata yote ya Kajana.

  • Ninahamasisha WanaParokia ya Kasumo kuwa na Bustani kubwa itakayozalisha miche ya miti ya Mbao, Kivuli, Dawa; na pia miti ya Matunda; na pia Mboga-mboga. Tumeanza kupanda miti mlima Gipfizi, kuona kama tunaweza hatimaye kupunguza athari ya uharibifu wa mazingira, na labda kufufua vijito vilivyokauka au vinavyoelekea kukauka.
  • Tutafanya linalowezekana kufanya mradi huu uwe si wa Kijiji cha Kasumo tu, bali Parokia nzima ya Kasumo.
  • Ni muhimu Serikali ikatusiaidia kuainisha vema mipaka ya Vijiji – ijulikane wazi na vizuri ili kupunguza uwezekano wa migogoro na migongano isiyo ya lazima. Tena serikali za vijiji, baada ya kubaini maeneo na mipaka ya vijiji vyao, watenge maeneo ya Mifugo na maeneo ya Kilimo ili kupunguza migogoro, na pia kudhibiti ufugaji holela hasa wa wageni wanaoweza kuvizia maeneo yetu na wingi wa mifugo yao.
  • Serikali isione aibu kuachana na msemo kwamba inawaletea wananchi maendeleo [kana kwamba wao – wananchi – wanaweza kukaa na kusubiri kuletewa] Badala yake iseme kuwa inawahamasisha kufanya kazi kujiendeleza, na pia kwamba inasaidia kuweka nyenzo za kazi na kuweka miundo-mbinu ambayo wananchi wakiitumia watapiga hatua ya maendeleo. Wananchi waelekezwe kufikiri kwamba watatumia miundo-mbinu na nyenzo zilizopo, au zitakazotolewa / kujengwa, na wanazoweza kujiundia wenyewe, ili kupiga hatua za kimaendeleo.
  • Buhigwe yetu ni nchi nzuri sana. Ni zawadi yetu toka kwa Mungu. Milima na mabonde yetu, watu wetu na mifugo yetu; Ardhi nzuri, mito na mabwawa yaliyosalia, hebu tuvitunze ili navyo hivyo vitutunze na tupate bado cha kurithisha Watoto na wajukuu wetu. Tuwe na moyo wa Ushindani: Tuwaze kuitengeneza Buhigwe kupiga hatua kubwa na ya haraka kuliko sehemu nyingine za Buha, nao baada ya miaka kumi waje kujifunza kwetu kitu / vitu fulani. Kwa mfano, nyumba zetu zipambwe na maua, na zizungukwe na miti ya matunda. Maeneo yetu yapendeze, maana maua si mali ya Mzungu au mkazi wa mjini tu. Tuishi katika maeneo na mazingira yanayovutia, yakiwa safi na salama.
  • Nchi au Chama Tawala vitakuwa na malengo yake. Tunayakaribisha. Lakini ni muhimu, au tuseme lazima Jimbo kama Buhigwe liwe na malengo yake pia. Vivyo hivyo na kila Kijiji kitakuwa na malengo yake pia, wakati kinatekeleza malengo ya kitaifa na ya Kijimbo.

 

Pd. Nzabhayanga Sebba, Agosti 25, 2020

Contact

Kigoma Green Revolution Organization [KGRO]

KGRO Head Office

Junction Road from Kasulu Town Council Office to Serengeti Hotel

P.O. Box 297

District: Kasulu

Ward: Murusi

Region: Kigoma.

Company Status: Non-Governmental Organization

Email Address: info@kgro.or.tz

Registration No: ooNGO/R/3141